Kivumbi kingine leo hii kwa Miamba wa Ligi 1 katika kundi la 4, hapa nawazungumzia Vinara wa kundi hilo dhidi ya Uingereza…. Hispania watawaalika Uingereza kwenye dimba la Benito Villamarin, Endapo Hispania akashinda leo basi atakuwa keshajihakikishia kucheza nusu fainali, huku Mwingereza naye akihitaji pointi 3 ili kurejesha matumaini ya kucheza nusu fainali pia.

Kocha Luis Enrique anaonekana kurejesha heshima ya wahispania baada ya timu hiyo mechi ya kirafiki juzi wakiinyuka Wales goli 4-1. Ikumbukwe kuwa Hispania haijafungwa kwenye michezo 27 ya mwisho iliyocheza huku wakiwa wameshinda mara 18 na kutoa sare mara 9…..Hispania pia ilishinda michezo yake yote miwili ya awali kwenye group hilo dhidi ya Croatia na Uingereza.

Uingereza naweza kusema kuwa bado hawajakaa vizuri toka warudi kutoka kombe la dunia kutokana na timu hiyo kutoshinda mechi hata mmoja katika michezo yake 4 ya mwisho ya ushindani. Kabla ya mchezo wa kwanza dhidi ya Hispania ulio malizika kwa Uingereza kufungwa 2-1 kwenye dimba la Wembley, uingereza ilikua imecheza michezo 24 kwenye Uwanja huo bila kupoteza.

Timu hizo mara 11 za mwisho kukutana Hispania ameshinda mara 6, sare 1 na Uingereza kashinda mara 4… Pia katika mara 26 za mwisho kukutana miamba hawa ni mechi 1 tu ilimalizika kwa sare ya bila kufungana.

Magoli 2 aliyofunga Paco Alcacer dhidi ya Wales yatafanya aendelee kuwa mchezaji wa kuchungwa kwenye mchezo huu endapo atacheza… Alcacer amefunga goli 8 kwenye michezo 5 ya mwisho aliyocheza kwenye klabu na timu ya taifa.

Harry Kane michezo 6 ya mwisho akiwa na timu ya taifa ameshindwa kuifunga goli hata moja, hii ni mara ya kwanza kwa Kane kucheza mda mrefu bila kufunga akiwa na timu ya Taifa.

Hispania mechi 27 za mwisho wamefunga jumla ya magoli 80, huku Uingereza ikiwa haijazidisha goli zaidi ya moja kwa mechi katika mechi zake 5 za mwisho.

Mchambuzi wetu Joseph Joseph alielezea kuwa Uingereza kwa sasa imepoteza hamasa sana tofauti na Hispania ambao wamekuwa na morali upya hasa baada ya Uteuzi wa kocha Luis Enrique…. “Hispania wananafasi ya kushinda mchezo huu ukizingatia watakuwa nyumbani ambapo ni ngumu wao kupoteza na pili wakishinda mchezo huu wanakuwa wameshatinga hatua ya Nusu fainali ya michuano hiyo ya UEFA NATIONS LEAGUE” alielezea.