Jini Mkata Kamba Asambalatisha Penzi la Linah na Baba Mtoto Wake
UBUYU hauchagui ni sehemu gani mtu akae ili aumung’unye, hata ukitembea, ukikaa, ukilala twende kazi tu! Ubuyu mtamu wa kumun’gunya leo ni wa mwanamuziki maarufu wa kike wa Bongo Fleva, Estalina Sanga ‘Linah’ au ‘Ndege Mnana’. Linah anadaiwa kuachana na mzazi mwenzake aliyetajwa kwa jina moja la Mchomvu ambaye amezaa naye mtoto mmoja wa kike aitwaye Tracy.
PENZI LIMEOTA MBAWA?
Penzi la wawili hao linadaiwa kuota mbawa wakati wakiwa kwenye taratibu za kufunga ndoa. Kwa mujibu wa mleta ubuyu wetu, Linah na mzazi mwenzake walianza kuingia kwenye mgogoro baada ya mwanadada huyo kujifungua mtoto wake huyo. Ilisemekana kwamba, mara kadhaa wamekuwa wakikalishwa chini na kuyamaliza mambo yao kichinichini bila mtu yeyote kujua kisha wanaendelea na uhusiano kama kawaida.
NI BAADA YA LINAH KUJIFUNGUA
“Unajua Linah na mzazi mwenzake walianza mgogoro wao kidogokidogo muda mfupi baada ya Linah kujifungua, lakini mara nyingi walikuwa wakikalishwa na kumaliza tofauti zao,” alisema mtoa ubuyu huop. Mpashaji wetu huyo alisema baada ya kuendelea kuishi huku tayari wakiwa kwenye mikakati ya kuoana, mgogoro kati yao ulizidi kuchipuka hadi kufikia hatua ya kuamua kila mmoja kuchukua hamsini zake na kubaki na jukumu la kulea mtoto wao.
NDIYO MAANA…
“Sasa hivi ndiyo maana unamuona Linah anajiachia sana tofauti na zamani alipokuwa na mzazi mwenzake. Sasa hivi siyo ajabu kumuona akikatika kama anavyofanya kwenye mitandao ya kijamii,” kilisema chanzo hicho. Chanzo hicho kilibainisha kuwa, wawili hao walishafikia hatua za karibu kabisa za kuoana na hata pete ya uchumba walikuwa wameshavalishana, kilichokuwa kikisubiriwa ni ndoa tu na hata mwanaume huyo ndiye aliyekuwa amemfungulia studio kubwa iliyopo maeneo ya Tegeta jijini Dar huku akimpa kila kitu.
“Sidhani kama kuna kitu Linah alikuwa anakosa kutoka kwa mwanaume wake huyo kwa sababu alikuwa akimpenda sana na tena alivyomzalia mtoto, mapenzi yalizidi kuongezeka kiasi ambacho baadhi ya watu walianza kuwaonea hata wivu,” kilisema chanzo.
NI WIVU
Mpashaji wetu aliweka wazi kuwa ugomvi wa wawili hao mara nyingi ulikuwa ni wivu wa kimapenzi hivyo hicho ndicho kilichosababisha uchumba wao huo kuvunjika ambapo mpaka sasa kila mmoja anamuona mwenzake mchungu.
“Hakuna cha zaidi kilichovunja uchumba ni wivu tu ndiyo ulikuwa ukiwatafuna wote wawili mpaka kufikia hatua ya kuvunjika kwa penzi lao,” alisema mpashaji huyo.
MSIKIE LINAH
Baada ya kulambishwa ubuyu huo, Ijumaa Wikienda lilimtafuta Linah ambapo mambo yalikuwa hivi;
Ijumaa Wikienda: Vipi Linah unaendeleaje?
Linah: Salama…
Ijumaa Wikienda: Vipi kuhusu ndoa yako na mzazi mwenzako maana naona kama siku zimepita na mlikuwa kwenye taratibu hizo?
Linah: Hivi kwani ukizaa na mtu mpaka muoane?
Ijumaa Wikienda: Una maana hamko pamoja tena?
Linah: Yaani ni hivyo tu sitaki kuongea zaidi.
Ijumaa Wikienda: Haya shukurani sana.
Linah: Asante.