MKUU wa Wilaya ya Ilala Sophia Mjema ameagiza Ofisa wa Kupambana na Rushwa TAKUKURU Ilala kufanya uchunguzi katika soko la samaki Feri katika Zoni namba tatu na zoni namba tano .

Mkuu wa Wilaya ya Ilala Sophia Mjema ametoa tamko hilo Dar es Salaam katika ziara yake ya kutatua kero za wananchi wa Wilaya hiyo na kusikiliza changamoto zao.

“Nakuagiza Ofisa TAKUKURU Ilala kuanzia sasa fanya uchunguzi katika zone namba tatu kama kuna ubadhilifu wowote  wahusika wapelekwe mahakamani pamoja na zone namba tano halafu ulete majibu kuna changamoto mbalimbali zinazohusiana na fedha za wananchi “alisema Mjema.

Alisema ziara ya soko la samaki  Feri ni maalum kwa ajili ya kuzungumza na wafanyabiashara wa soko hilo ambapo kila Mkuu wa idara anatoa ufumbuzi wa kero yake.

Aliwataka watendaji wake wa Ilala  kufanya kazi kwa weledi kila mtu kusimamia majukumu yake sambamba na utatuzi wa kero za wananchi.

Wakati huo huo Mkuu wa Wilaya Sophia Mjema ameagiza Meneja wa Benki ya Dar es Saalam Benki DCB kesho Jumanne Octobar 16  asubuhi afike Ofisi ya Mkuu wa Wilaya kutoa maelezo kwanini Benki ya DCB imechelewa kutoa  mikopo isiyo na riba kwa wananchi wa Wilaya ya Ilala.

“Nakuagiza Katibu Tawala Wilaya ya Ilala mpigie simu Mkurugenzi wa DCB Benki aje atoe maelezo  kwa   kuchelewa kuwapa mikopo Wanawake na Vijana isiyo na riba  Benki yake ndio ilipewa jukumu hilo toka awali na serikali ilishatoa maelekezo”.alisema.