RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Ali Mohamed Shein amesema kwamba maonyesho ya Utalii yanayofanyika Zanzibar ni muhimu kwa Serikali na wananchi kwa kuwa yamelenga kuitangaza Zanzibar na sekta ya utalii ambayo ndio muhimili mkuu wa uchumi.

Dk. Shein ameyasema hayo leo katika viwanja vya hoteli ya Verde, Mtoni Mjini Zanzibar katika ufunguzi wa maonyesho ya Utalii Zanzibar ya mwaka 2018 ambayo yalihudhuriwa na viongozi mbali mbali wakiwemo Makamu wa Rais Samia Suluhu Hassan, Makamu wa Pili wa rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Idd, wadau wa utalii na viongozi mbali mbali wa vyama vya siasa na Serikali pamoja na wananchi.

Katika maelezo hayo, Rais Dk. Shein alisema kuwa Utalii umekuwa ukichangia asilimia 27 kwa Pato la Taifa na asilimia 80 ya fedha za kigeni zinazokusanywa ambapo muda wanaokaa watalii nchini umeongezeka ambapo hivi sasa mtalii hutumia wastani wa siku 8 badala ya 6 kama ilivyokuwa miaka 5 iliyopita.

Rais Dk. Shein alieleza juhudi mbalimbali za kuimarisha utalii zinazoendelea kuchukuliwa na Serikali zikiwemo kuanzisha mpango wa “Utalii kwa wote” ambapo lengo kuu la mpango huo ni kuhakikisha kwamba sekta ya utalii inawanufaisha wananchi wote wa Zanzibar na kuimarisha ustawi wa wananchi kwa jumla.

Alieleza imani yake kwamba maonyesho hayo ni njia bora na madhubuti ya kuitangaza Zanzibar pamoja na fursa mbali mbali zilizopo za kiuchumi kwa wawekezaji.

Aidha, Rais Dk. Shein aliiagiza Wizara ya Habari, Utalii na Mambo ya Kale kuhakikisha kuwa watu wanaotembeza wageni wawe wamepatiwa mafunzo yanaayostahiki, wawe na vibali na wahakikiwe kila baada ya muda ili kuhakikisha kwamba hawaharibu historia ya Zanzibar kwa kuisimulia isivyo au kwa kuzingatia matakwa na utashi wao binafsi.