Uongozi wa makampuni ya ‘MeTL’ unaomilikiwa na mfanyabiashara maarufu nchini, Mohamed Dewji umekanusha taarifa za uvumi juu ya kusitisha shughuli za uzalishaji kwenye makampuni yake kufuatia tukio la kupotea kwa mmiliki wake Alhamisi ya wiki iliyopita.

Taarifa za kusitishwa kwa uzalishaji wa makampuni hayo zilianza kusambaa hivi karibuni kupitia mitandao mbalimbali ya kijamii, zikiinukuu uongozi wake juu ya azma yake ya kusitisha uzalishaji ifikapo Oktoba 20 mwaka huu.

Kupitia mitandao yake ya kijamii, MeTL imeandika, “tunaendelea kusikitishwa na tukio lililomtokea Afisa Mtendaji Mkuu wa kampuni yetu, Mohammed Dewji. Pia tunapenda kutoa taarifa kwamba taarifa zinazosambaa katika mitandao ya kijamii kuwa tarehe 20/10/2018 tutasimamisha shughuli za uzalishaji katika makampuni yetu siyo za kweli.”

Mohamed Dewji alitekwa na watu wasiojulikana Alhamisi ya wiki iliyopitana mpaka sasa hakuna taarifa rasmi za kupatikana kwake licha ya Jeshi la Polisi kuwashikilia na kuwahoji watu 26.