Wakati Katibu wa Itikadi na Uenezi wa Chama cha Mapinduzi (CCM) akiwa ametangaza kuwa mwisho wa kufanyika kwa chaguzi ndogo za marudio ni Disemba 2018, tume ya taifa ya uchaguzi (NEC) imesema kuwa muda bado upo kwa mujibu wa katiba.

Mkurugenzi wa uchaguzi wa tume ya taifa ya uchaguzi, Dkt. Athuman Kihamia amesema kuwa uchaguzi wa marudio huwa unafanyika kwa mujibu wa katiba na husitishwa pindi muda utakapokuwa umefika kikomo.

Dkt. Kihamia amesema kuwa kuwa muda wa kufanyika kwa uchaguzi mdogo bado upo hadi miezi kumi na mbili kabla ya Bunge kuvunjwa ambapo kikomo kitakuwa mwezi Julai 2019.

“Kisheria muda unaruhusu bado kufanya chaguzi za marudio, hakuna muda maalum isipokuwa muda uliowekwa na katiba ukifika ukomo”,amesema Dkt. Kihamia.

Jana Oktoba 18, Makamu Mwenyekiti wa NEC, Jaji wa Mahakama ya Rufaa, Mbarouk Salum Mbarouk ametangaza uchaguzi mdogo kwenye majimbo mawili na kata 26 za Tanzania Bara ambapo utafanyika Disemba 2, 2018 katika majimbo ya Babati Mkoani Manyara na Ukerewe jijini Mwanza, ambapo uchaguzi huo utafanyika sambamba na uchaguzi wa jimbo la Simanjiro na Serengeti pamoja na kata 21 za Tanzania Bara uliotangazwa awali.

Uchaguzi huo unafanyikiwa ikiwa tayari, Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Humphrey Polepole akisema kuwa wabunge wa upinzani wanaotaka kujiunga na chama hicho mwisho wa kufanya hivyo ni Disemba 2018, hivyo unadhaniwa kuwa ni uchaguzi wa mwisho wa marudio kwa chama hicho hadi mwaka 2020 uchaguzi mkuu utakapoitishwa.

Polepole alitoa kauli hiyo Oktoba 7, 2018 kupitia ukurasa wake wa twitter ambapo aliandika,“Tumezingatia na tunaweka jitihada zetu zote katika kushughulika na utatuzi wa shida za watu wetu wa Tanzania. Mwaka 2018 ndiyo mwisho kwetu kufanya chaguzi ndogo za ubunge kwa wale wanaohama vyama vyao na kujiunga na CCM. Watakaoikosa raundi hii mbaki hukohuko tutakutana 2020”.