Baadhi ya maofisa wa Mamlaka ya Mapato mkoani Kilimanjaro (TRA), wanadaiwa kutoa lugha za vitisho na kauli zisizopendeza kwa wafanyabiashara wakati wa ukusanyaji kodi, ‘zimemchefua’ Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan na kuonya waache mara moja.

Samia yuko mkoani Kilimanjaro kwa ziara ya siku tano, kwa ajili ya kufungua na kukagua miradi mbalimbali ya maendeleo kuanzia Novemba 9 hadi 13 mwaka huu.

“Vipo vikundi vya watu vinavyofika kwa wafanyabiashara vikisema vimepewa amri kutoka juu kukusanya kodi, sisi hatujawatuma kuwanyanyasa (wafanyabiashara) ili wapate mapato na badala yake tumewaagiza wawashawishi wafanyabiashara kuona umuhimu wa kulipa mapato kwa jili ya maendeleo ya nchi yao,

“Inasikitisha, baadhi ya watendaji wa TRA wamekuwa wakifika kwa wafanyabiashara na badala ya kutumia lugha nzuri ya kumshawishi mfanyabiashara kulipa kodi, wao wamekuwa wakitumia lugha chafu na maneno ya vitisho.”