TAARIFA kuhusu baadhi ya maofisa wa Mamlaka ya Mapato mkoani Kilimanjaro (TRA), kudaiwa kutoa lugha za vitisho na kauli zisizopendeza kwa wafanyabiashara wakati wa ukusanyaji kodi, ‘zimemchefua’ Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan na kuonya waache mara moja.

Samia yuko mkoani Kilimanjaro kwa ziara ya siku tano, kwa ajili ya kufungua na kukagua miradi mbalimbali ya maendeleo kuanzia Novemba 9 hadi 13 mwaka huu.

“Vipo vikundi vya watu vinavyofika kwa wafanyabiashara vikisema vimepewa amri kutoka juu kukusanya kodi, sisi hatujawatuma kuwanyanyasa (wafanyabiashara) ili wapate mapato na badala yake tumewaagiza wawashawishi wafanyabiashara kuona umuhimu wa kulipa mapato kwa jili ya maendeleo ya nchi yao,

“Inasikitisha, baadhi ya watendaji wa TRA wamekuwa wakifika kwa wafanyabiashara na badala ya kutumia lugha nzuri ya kumshawishi mfanyabiashara kulipa kodi, wao wamekuwa wakitumia lugha chafu na maneno ya vitisho.”

Makamu wa Rais, alisema ni kweli serikali inataka ongezeko la mapato, lakini hawapo tayari kuona wafanyabiashara wakinyanyasika wakati wa ukusanyaji wa kodi, zaidi ya kupewa elimu ya kutosha kwa nini wanapaswa kulipa kodi na wapate kuhudumiwa kwa wakati.

Katika sekta ya afya, Samia ameeleza kutoridhishwa kwake na kiwango cha watoto 600 kufa kwa kukosa lishe bora, kati ya mwaka 2017/2018, huku kukionekana kuwepo kwa upungufu wa vifo vya mama na mtoto.

Alisema watoto hao waliopoteza maisha kutokana na kukosa lishe bora, ni watoto wenye umri chini ya miaka mitano.

“Wakina mama wenzangu wa Kilimanjaro, acheni kutumia wakati mwingi kutafuta pesa na rasilimali, badala yake wekezeni zaidi kwenye watoto, kwani hili ni taifa la kesho. Naagiza pia ustawi wa jamii hakikisheni mnafutalia changamoto hii kwa haraka,”alisisitiza Makamu wa Rais.

Kuhusu tatizo la ajira, Makamu wa Rais, alimtaka Mkuu wa mkoa wa Kilimanjaro, Dk. Anna Mghwira kuchagua chuo kimoja cha ufundi mkoani hapa ambacho kitatoa elimu hiyo kwa kundi kubwa la vijana watakaohitajika kama nguvu kazi ya sekta ya viwanda nchini.

“Vijana wengi wa sasa wanapomaliza vyuo vikuu wanaweka mawazo yako katika kuajiriwa jambo ambalo siyo sahihi na wale wanapata zile nafasi hawazitumii ipasavyo hali ambavyo imeonekana hakuna matokeo chanya yanayoweza kujitokeza… Vijana onyesheni moyo wa kufanya kazi na kuipenda kazi … jitumeni na muache kupoteza muda mwingi kwenye mitandao ya kijamii,” alieleza Samia

Awali, akisoma taarifa ya mkoa huo kwa Makamu wa Rais, Dk.Mghwira aliiomba serikali kuangalia namna ya kuongeza nguvu kwa Taasisi ya Maendeleo ya Viwanda ya KIDT ambayo ina uwezo mkubwa wa kutengeneza vipuli vitakavyotumika nchi nzima kwa ajili ya umeme.