Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan amewataka Watumishi wa Serikali Wilayani Rombo kufanya kazi kwa kushirikiana.

Makamu wa Rais ameyasema hayo leo mara baada ya kupokea taarifa ya Wilaya hiyo kutoka kwa Mkuu wa Wilaya,  Agnes Hokororo.

“Wote tunajenga nyumba inayoitwa Tanzania katika nafasi yako yoyote ulipo unajenga nyumba inayitwa Tanzania, kwa itikadi yako yoyote uliyonayo unajenga nyumba inayoitwa Tanzania tunatawaliwa na sheria moja, tunataliwa na miongozo hiyo hiyo ya Serikali, kanuni na mambo mengine na hiyo hiyo Serikali”.

Katika ziara yake Wilayani Rombo Makamu wa Rais alikagua maendeleo ya mradi wa ujenzi wa Jengo la Utawala la Halmashauri ya Rombo, mradi wa maji Shimbi Mashariki,kukagua shamba la Miti Rongai.

Makamu wa Rais ambaye yupo kwenye ziara ya kukagua na kuhamasisha shughuli za maendeleo pia alipata nafasi ya kuwasalimu wananchi wa Tarakea waliojitokeza barabarani kumsalimia na alihutubia mkutano wa hadhara katika viwanja vya shule ya msingi Keni-Mengeni.

Kwa upande mwingine Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais TAMISEMI, Selemani Jafo amesema kuwa Serikali hii inafanya jambo la kihistoria kwa kukamilisha ujenzi wa vituo vya Afya 350.