Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Kangi Lugola amesema kamwe serikali ya Tanzania, haitaruhusu ushoga na kwamba kila kiungo kilichoumbwa na Mungu kwenye mwili wa mwanadamu kina kazi yake.

Kauli ya Lugola imekuja kufuatia Mbunge wa Jimbo la Konde (CUF), Khatibu Saidi Haji, kusema anashangazwa na serikali kuwa na kauli laini kuhusu vitendo vya ushoga lengo likiwa ni kubembeleza mikopo.

Akichangia mapendekezo ya mpango wa Maendeleo ya Taifa wa 2019/20, Haji amesema “kabla ya kuanza kuchangia, naanza na utangulizi ambao ni muhimu kwa ninavyoona katika siku za karibuni kumezuka mjadala kuhusiana na ndoa za jinsia moja, tumesikia kauli za mawaziri akiwamo Kangi Lugola, na Waziri wa Mambo ya Nje (Balozi Agustino Mahiga)”.

“Katika kauli zao inaoneka kuna kamtego juu ya kukubaliana na jambo hili na kukinzana na jambo hili, naomba niwaambie, iwe ni mtego ama ni bahati mbaya, sisi watanzania hatutaingia katika mtego wa ushoga, Tanzania hatutaki ushoga. Iwe mmetumwa ama ni mtego watanzania hatutakubali kuingia kwenye ndoa za jinsia moja”, amesema Haji.

Akijibu swali hilo Waziri Lugola amesema, “Msiseme kuwa labda serikali inajichanganya kwenye jambo hili, ni maelekezo ambayo tunatoa labda vyombo vinaripoti tofauti, lakini serikali yetu kamwe, Tanzania ni hekalu la roho mtakatifu. Hatuwezi kukubali hekalu la roho mtakatifu likatumika kwa mambo ambayo hayakubaliki,” amesema Lugola.

Katika mkutano wake na waandishi wa habari Oktoba 31, 2018, Makonda alitangaza kampeni ya kukabiliana na vitendo vya ushoga katika jiji la Dar es salaam, ambapo aliunda kamati ya watu 15 kwa ajili ya kupambana na wanaojihusisha na ushoga, wanaotapeli wengine kwa kutumia mitandao wakijifanya ni viongozi maarufu nchini.

Baadaye Novemba 4, Wizara ya Mambo ya nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki ilitoa msimamo wake juu ya sakata la Mkuu wa Mkoa wa Dar es saalam dhidi ya ushoga katika mkoa wake  nakudai kuwa ni mawazo yake na si msimamo wa serikali.

Huku Novemba 7, katika mkutano wake na vyombo vya habari, Waziri wa mambo ya ndani ya nchi Kangi Lugola amewahakikishia usalama watu wanaojihusisha na mapenzi jinsia moja nchini (Mashoga) na kwamba hakuna atakayewakamata.