Mkuu wa Wilaya ya Dodoma Mjini, Patrobasi Katambi amezungumzia mahusiano yake na Mwenyekiti wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo CHADEMA, Freeman Mbowe na kusema atakuwa na mahusiano mazuri na kiongozi huyo kama ataamua kuunga mkono maendeleo ya Tanzania.

Katambi ametoa kauli hiyo wakati akizungumza na kituo cha EATV alipokuwa akifanya mahojiano maalum juu ya mahusiano yake na mwenyekiti wa zamani wa chama chake ambaye kwa sasa yuko gerezani baada ya kufutiwa dhamana dhidi ya kesi inayomkabili pamoja na viongozi wenzake wa CHADEMA.

Nitaendelea kuwa na mahusiano na kila mtu aliyekuwa anaitakia mema Tanzania hii, lakini kama haendani na kuangalia maslahi ya wengi huyo mimi atakuwa ni adui yangu, ili uweze kujua nina mahusiano mazuri au mabaya na (Mbowe) angalia hivyo vitu, zaidi ya hapo yatabaki mahusiano kwa sababu ni mtanzania.”

Hivi karibuni Kada huyo wa zamani wa CHADEMA ambaye pia alikuwa Mwenyekiti wa Baraza la Vijana la chama hicho alieleza kuwa “sijawahi kuvisema vibaya (vyama vya upinzani) ila nilikuwa nasema ukweli, kwa sababu walikuwa wanalalamikia kuhusu tume huru ya uchaguzi ili waweze kuwathibitishia watanzania wajiuzulu ubunge wao, na nafasi nyingine za kisiasa ili tujue walipatikana kwa tume haramu, madai yao kwa sasa ni kupinga maendeleo lakini sisi tulifanya kisayansi,”

Kuhusu Nape Nnauye na Bashe, wao walikuwa wanazungumzia kuhusu maendeleo ya nchi lakini wabunge wa upinzani wengine ni vibaraka kwa sababu walikuwa wanapinga maendeleo,” ameongeza.

Aidha Katambi alikanusha madai ya kufanya udhalilishaji kwa baadhi ya watuhumiwa wa makosa ya kiuhalifu ambao amekuwa akiwakamata kwenye wilaya yake ya Dodoma Mjini.