Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya makazi, William Lukuvi amewataka wananchi wa Kijiji cha Mapogolo mkoani Iringa kuacha kuuza ardhi kiholela kwasababu hali hiyo inaweza kusababisha ongezeko la umasikini kutokana na wananchi kukosa ardhi kwa ajili ya kilimo.

Kauli hiyo ya Waziri Lukuvi imekuja kufuatia madai ya kuwepo kwa idadi kubwa ya wakazi wa kijiji cha mapogolo kutegemea shuguli za kilimo na ufugaji lakini wamekuwa wakikwama kwasababu wakulima hao wamekuwa na tabia ya kuuza ardhi yao bila mpangilio.

Akizungumza wakati wa hafla ya kutoa hatimiliki za Kimila kwa wakazi 2,204  wa  kijiji cha Mapogolo Waziri Lukuvi amesema upimaji wa ardhi na  ugawaji wa hati hizo umesaidia kupunguza migogoro ya ardhi kwa wananchi.

Upangaji na upimaji wa ardhi ni jambo la msingi tunalosimamia kwa sababu linatusaidia kupungunza migogoro, baina ya wananchi kwa wananchi lakini kubwa zaidi itawaongezea thamani ya ardhi, kwa hiyo niwasihi ndugu zangu msipende kuuza ardhi kiholela

Hati hizo 2,204  zimetolewa na mradi wa urasimishaji ardhi vijijini  chini ya ufadhiri wa ‘feed the future’ chini ya mpango wa kupunguza njaa na Utapiamlo kwa ufadhiri wa Shirika la Maerndeleo la Kimataifa la Marekani USAID kwa lengo la kumaliza migogoro ya ardhi na kuwainua kiuchumi wananchi.