Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Amri Jeshi Mkuu, Dkt. John Magufuli ametoa salamu za Kumbukumbu ya Miaka 57 ya Uhuru wa Tanzania Bara, leo Ijumaa, Desemba 7, 2018 Ikulu jijini Dar es Salaam.

Akituma salam hizo, Rais Magufuli kwa mujibu wa Ibara ya 45 Ibara ndogo ya 1 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ametangaza msamaha kwa wafungwa 4,477 waliyokuwa wamefungwa / kuhukumiwa kwenye magereza mbalimbali nchini ambapo  kati yao 1,176 wataachiwa Desemba 9, 2018 katika Sikukuu ya Uhuru.

Msamaha huo wa Rais Dkt. Magufuli utawahusu wagonjwa, wazee walio na umri zaidi ya miaka 70, wanawake wajawazito,wanaonyonyesha, wenye watoto wadogo, walemavu wa mwili na akili,

Aidha amesema kuwa msamaha huu hautawahusu wafungwa wenye adhabu ya kifungo cha maisha, adhabu ya kunyongwa, wenye makosa kama biashara ya dawa za kulevya, kukutwa na viungo vya binadamu,makosa ya silaha ama mlipuko wowote, makosa ya kunajisi,shambulio la aibu,

kuwapa mimba wanafunzi wa shule za msingi na sekondari, kuhujumu uchumi, rushwa, ujangili, wafungwa wote waliowahi kupata msamaha wa Rais kwa kutumikia nusu ya adhabu kifungo, waliowahi kufungwa na kurudi tgena gerazeni, wenye makosa ya kinidhamu ndani ya gereza na wote walioanza kutumia kifungo chao kuanzia Desemba mosi 2018.

“Ninawatakia Watanzania wote kila la heri katika Maadhimisho ya Miaka 57 ya Uhuru wa Tanzania Bara, tusheherekee kwa amani, Mungu wabariki Watanzania wote, Mungu ibariki Tanzania, Mungu ibariki Afrika.” amesema Rais Magufuli.

Aidha, Magufuli amesisitiza kuwa fedha iliyotengwa kwa ajili ya sherehe za Uhuru Desemba 9 mwaka huu, itatumika kujenga Hospitali mpya ya Uhuru jijini Dodoma.