Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Magufuli amesema kuwa Uhuru uliopatikana Disemba 9, 1961 ni mwanzo wa kutafuta Uhuru wa kiuchumi ambao ameutaja kuwa ndio mgumu zaidi kupatikana.

Rais Magufuli ametoa kauli hiyo leo, Ikulu jijini Dar es salaam wakati akitoa salamu za Kumbukumbu ya miaka 57 ya Uhuru ikiwa taifa linaelekea kwenye maadhimisho ya siku hiyo hapo Desemba 9.

Rais Magufuli amesema kuwa; “Katika kuadhimisha miaka 57 ya Uhuru wa Tanzania Bara, basi nimeagiza fedha zilizokuwa zitumike kuadhimisha siku hiyo, zikajenge hospitali itakayoitwa ‘Uhuru hospital’ jijini Dodoma“.

Ameongezea kuwa, “Watu wengi wameshahamia Dodoma, hii imefanya mahitaji ya huduma za kijamii ikiwemo Afya jijini humo kuongezeka, hivyo tumeamua kujenga hospitali nyingine kubwa itakayosaidiana na hospitali ya Mkapa iliyopo UDOM na hospitali ya Mkoa wa Dodoma“.