Wamachinga jijini Mbeya wametekeleza agizo la Mkuu wa mkoa huo Albert Chalamila la kuvunja vibanda vyao walivyojenga nje ya soko la kuu la Mwanjelwa kabla ya saa 10:00 jioni leo.

Agizo hilo la Wamachinga wa soko la Mwanjelwa na kituo cha mabasi cha Kabwe kuondoa vibanda vyao, lilitolewa hili karibuni na mkuu wa mkoa na kusisitizwa na Mkurugenzi mtendaji wa jiji la Mbeya SSP James Kasusura.

Mpaka sasa wamachinga hao wanaendelea kubomoa wenyewe vibanda vyao vilivyoko nje ya soko hilo na kuhamia ndani ambako wanatakiwa kupanga vyumba ndani ya soko hilo na kufanya biashara zao kwa uhuru.

Akiongea na wanahabari Desemba 5, 2018 Mkurugenzi huyo mtendaji wa Jiji, aliwataka wamachinga kuchukua vymba ndani ya soko la Mwanjelwa ama kuhamia soko la nane nane ambalo ndio limejengwa maalum kwaajili yao.

Imeelezwa kuwa katika soko la Mwanjelwa serikali ya mkoa imepunguza kodi ya vyumba kutoka shilingi 750,000 hadi 150,000 kwa vyumba vya chini, vyumba vya kati kutoka 250,000 hadi 50,000 na vyumba vya juu kutoka 150,000 hadi 30,000.