Klabu ya soka ya Simba imethibitha tarehe ya mchezo wake wa raundi ya kwanza, hatua ya kwanza ya klabu bingwa Afrika dhidi ya Nkana FC ya Zambia ambao utapigwa Jumamosi Desemba 15, 2018.

Mbali na kuthibitisha tarehe, Simba pia imetangaza kuandaa utaratibu wa mashabiki wake wanaotaka kusafiri kwenda nchini Zambia kuiunga mkono timu yao kwenye mchezo huo.

”Tumeandaa utaratibu  wa  Safari kwa njia ya barabara ambapo nauli  ni  shilingi  laki  moja  na  elfu thelathini   (130,000)   kwenda   na   kurudi, kutokea Dar   es   Salaam   hadi mjini Kitwe na  safari itaanza Alhamisi Alfajiri na  kufika  huko Ijumaa jioni” imeeleza taarifa ya klabu.

Pamoja  na  nauli hiyo, msafiri  pia anapaswa kuwa  na  hati  ya kusafiria  inayokidhi  matakwa ya kisheria na Hati ya chanjo ili aweze kusafiri kwenda Zambia.

Simba inakutana na Nkana Red Devils baada ya kuitoa Mbabane Swallos kwa jumla ya mabao 8-1 katika michezo miwili ya raundi ya awali ya michuano hiyo. Simba ikivuka hatua hii inaingia katika hatua ya makundi.