Tuzo kubwa za muziki duniani ‘Grammy’, zimetoa orodha ya ‘Nomination’ ya wasanii na kazi zao zilizoingia kwenye kinyang’anyiro, huku muziki wa Reggae nao ukipewa kipengele chake cha ‘Best Reggae album’ kama ilivyo kawaida kwa tuzo hizo.

Licha ya kwamba muziki wa Reggae  hivi karibuni umeandika historia mpya ya kutambuliwa na Umoja wa Mataifa kama urithi wa utamaduni wa dunia na ambao unapaswa kulindwa, umeingiza album tano kwenye tuzo za Grammy, huku ikitafutwa moja tu ambayo itaweza kunyakua tuzo hiyo.

Album hizo ni  ‘As the world turns’ ya Black uhuru, ‘Reggae forever’ ya Etana, ‘Rebellion rises’ ya Ziggy Marley, ‘A matter of time’ ya Protoje na ’44/876′ ya Sting na Shaggy.

Katika Album hizo tatu miongoni mwao ndio zimekuwa zikitajwa sana na watu, ikiwemo ya Rebbelion rises ya Ziggy Marley, Reggae forever ya Etana na 44/879 ya Sting Swahiba wake Shaggy.

Iwapo Ziggy Marley atachukua tuzo hiyo basi atakuwa anabeba Gramy kwa mara ya nane, jambo ambalo, halikuwahi kutokea kwa baba yake mzazi Robert Marley, licha ya jitihada zote alizofanya kwenye muziki wa Reggae wakati wa uhai wake.

Bob Marley hakuwahi kushinda  tuzo ya Grammy na badala yake alipewa tuzo ya heshima kwa kazi zake za muziki zilizosambaa dunia nzima.

Tuzo hizo za mwaka huu ambazo ni za 61, zitafanyika Februari 10, 2019 nchini Marekani, ambapo jumla ya vipengele 84 vitapata washindi.