Waziri wa Mifugo na Uvuvi,Luhaga Mpina ametangaza neema kwa wafugaji kwa kugawa ekari 972, 500 za ardhi ajili ya wafugaji wanaotangatanga kutafuta malisho ya mifugo yao ili kupata ufumbuzi wa kudumu ambao utamaliza kabisa migogoro baina ya wafugaji na wakulima iliyodumu kwa miaka mingi na kusababisha uvunjifu wa amani.

Akizindua zoezi la ugawaji wa ardhi hizo kwa wafugaji nchini katika Ranchi ya Kalambo wilayani Nkasi mkoani Rukwa, Waziri Mpina amesema uamuzi huo wa Serikali umekuja kufuata wafugaji wengi nchini kuhangaika kila mahali kutafuta malisho na kusababisha migogoro mingi baina ya wafugaji, wakulima na watumiaji wengine wa ardhi.

“Pia wafugaji wengi walipata harasa kubwa kwa mifugo yao kutaifishwa kutozwa faini kubwa na hata mingine mingi kufa kutokana na kukamatwa kisha kushikiliwa kwa muda mrefu bila huduma muhimu ikiwemo maji, malisho na matibabu kwenye hifadhi mbalimbali za taifa nchini.”Alisisitiza Mpina

Alisema hadi sasa ekari 25,000 zenye uwezo wa kuhifadhi mifugo 6,000 katika Ranchi ya Kalambo
mkoani Rukwa wafugaji zimemegawiwa ambapo na jumla ya ng’ombe 3,000 wameshaingia kwenye ranchi hiyo wakati Serikali na wafugaji wenyewe wakiendelea kutafuta suluhisho la kudumu la kupata malisho.

Amewataka wafugaji wote wanaohangaika kutafuta malisho kutumia fursa hiyo iliyotangazwa na Serikali ya uwepo wa maeneo kwa ajili ya kulishia mifugo ili wawe karibu pia huduma za tiba na chanjo pindi mifugo yao inapopata maradhi.

Akiwa katika mkutano wa pamoja baina ya Rachi ya Kalambo na wawekezaji Waziri Mpina
alipongeza Timu maalum aliyoiunda ya kutatua migogoro ya wafugaji na watumiaji wengine wa ardhi kwa kufanikisha zoezi la upimaji na ugawaji wa ardhi hiyo kwa wafugaji pamoja na kutatua migogoro yote iliyokuwepo baina ya wafugaji na watumiaji wengine wa ardhi katika mikoa ya Rukwa, Katavi na Kigoma.

Aidha ailiiagiza Timu hiyo kuhakikisha kwamba inazunguka nchi nzima kwenye migogoro na kuitatua ili kuboresha mifugo iweze kuchangia katika viwanda hapa nchini.

Pia alimwagiza Katibu Mkuu Mifugo kuhakikisha ukaratabi wa kituo cha uchunguzi wa magonjwa ya wanyama cha Kanda ya Kusini Magharibi kinakamilika ifikapo Februari mwakani ili kutokana na mikoa ya Katavi, Rukwa kutokuwa na kituo hicho licha ya kuwepo mifugo mingi.

Kaimu Mkuu wa Mkoa wa Rukwa, Dk Halfan Haule alisema kutokuwepo kwa maeneo ya malisho na maji ya kutosha kwa ajili ya mifugo kumekuwepo na migogoro kati ya wafugaji na watumiaji wengine wa ardhi na kumshukuru Waziri Mpina kwa uamuzi wa kugawa vitalu kwa wafugaji.

Alisema Mkoa wa Rukwa umekuwa ukikabiliwa na magonjwa ya mifugo ikiwemo homa ya nguruwe(ASF), Homa ya Mapafu ya Ng’ombe(CBPP), Homa ya mapafu ya mbuzi(CCPP), Ugonjwa wa miguu na midomo(FMD), Ugonjwa wa mapele ngozi(LSD), Ugonjwa wa kichaa cha mbwa na ugonjwa wa mdondo(ND).